TU WARITHI KWA MUNGU PAMOJA NA KRISTO.
Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu katika Kristo Yesu.
Roho wa Mungu anakaa ndani yetu, hivyo hatuufuati mwili, bali tunaifuata roho. Na wote tunaoongozwa na Roho wa Mungu, ndio wana wa Mungu. Hatukupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu, bali roho ya kufanywa wana, na kwa hiyo twalia Aba, yaani Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kuwa sisi tuu watoto wa Mungu; hivyo kama watoto, tu warithi wa Mungu, turithio pamoja na Kristo, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.
Basi sisi si watumwa tena bali tu wana, na kama wana tu warithi kwa Mungu. Tulikuwa chini ya sheria, tukakombolewa ili tupate hali ya kuwa wana; na kwa kuwa tumekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye Aba, yaani, Baba. Na kama sisi ni wa Kristo, tumekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.
Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Mungu, ametufanya imara katika Kristo, katutia mafuta na ametutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu. Basi tufahamu sana haya yasemwayo, maana Bwana atatupa akili katika mambo yote.
Warumi 8:17(9,14-17), Wagalatia 4:7,5,6,
Wagalatia 3:29, 2 Timotheo 1:7,
2 Wakorintho 1:21-22, 2 Timotheo 2:7.
Comments
Post a Comment