UMOJA TULIOITIWA ILI TURITHI BARAKA.
Neema na amani na ziongezwe kwetu.
Tuwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu; watu tusiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo tuliyoitiwa ili turithi baraka. Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila, Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana.
Tuwabariki wanaotuudhi; tubariki, wala tusilaani. Tufurahi pamoja nao wafurahio; tulie pamoja nao waliao. Tupatane nia zetu sisi kwa sisi. Tusinie yaliyo makuu, lakini tukubali kushughulishwa na mambo manyonge. Tusiwe watu wa kujivunia akili. Tusimlipe mtu ovu kwa ovu. Tuangalie yaliyo mema machoni pa watu wote. Tukae katika amani na watu wote. Tusijilipize kisasi, bali tuipishe ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.
Maneno yetu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu. Tumesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; Lakini Kristo anatuambia, tusishindane na mtu mwovu; lakini mtu atupigaye shavu la kuume, tumgeuzie na la pili. Atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo. Kristo pia anatuambia, tuwapende adui zetu, tuwaombee wanaotuudhi, ili tupate kuwa wana wa Baba yetu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.
Maana tukiwapenda wanaotupenda sisi twapata thawabu gani? Tena tukiwaamkia ndugu zetu tu, tunatenda tendo gani la ziada? Hata watoza ushuru na watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Tuwaonye wale wasiokaa kwa utaratibu; tuwatie moyo walio dhaifu; tuwatie nguvu wanyonge; tuwavumilie watu wote. Mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote tulifuate lililo jema, sisi kwa sisi na kwa watu wote. Kristo Yesu alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki.
Ni nani atakayetudhuru, tukiwa wenye juhudi katika mema? Tusishindwe na ubaya, bali tuushinde ubaya kwa wema. Basi hapo tutakuwa wakamilifu, kama Baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu.
1 Petro 3:8-11,13, Warumi 12:14-19,21, Mathayo 5:37-48,
1 Wathesalonike 5:14-15, 1 Petro 2:23.
Comments
Post a Comment